November 7, 2011

Ukitaka kujifunza kuogelea, ingia majini



Blogu hii ni uwanja wa mapambano. Vita kati yangu na jinamizi la kutisha—uvivu wa kuandika. Kila ukiona kuna kitu kipya kimeandikwa, ujue huo ni ushindi kwangu. Pengine wakati unaangaza macho  yako hapa, unaweza kuokota kito cha thamani ama kitu chenye ladha ya kukufaaa kula—kwa macho.

Wakati nafikiria kuanzisha blogu yangu majina kadhaa yalianza kujitokeza. Yenyewe, tu bila hata kuyaita: mkama special, kila kitu, mpyampya na kadhalika. Yote niliyakataa, bila sababu. Pengine sababu ya kuyakataa ni tabia yangu ya kutafuta mbadala- kwa karibu kila kitu.
Kwa  karibu miezi sita, hii blogu iliitwa kiporobaridiujimoto(neno moja).Hiyo ilikuwa ni baada ya kutafuta mbadala wajina-kiporobaridinaujimoto-ambalo lilidumu kwa siku mbili—sababu kazi za mshahara zilizidi nikakosa muda wa kuiwaza project yangu mpya.
Nafikiri umeanza kushangaa, miezi sita ya blogu na leo ndio naweka makala ya kwanza? Tafadhali rejea kauli yangu ya mwanzo—napambana na jinamizi kubwa jeusi kama usiku usio mbalamwezi. Laitwa uvivu wa kuandika.
Majuzi tu, nilialikwa na dada mmoja kwenye mkutano wa bloggers wa Dar es Salaam. Pernille alikua anafanya kazi dawati mkabala na mimi.  Naheshimu sana staili yake ya kuandika bidii yake. Aliponialika nikajishaua kuwa ninayo blogu.
“Unablogu kuhusu nini?” aliuliza. Jibu la swali hilo sikulitoa, kwa vile halipo. Ila nakumbuka niliongeaongea maneno ambayo, naamini aliyaelewa kwa kuwa hakuniuliza tena.
Niliishia tu kumfafanulia maana ya kiporo baridi uji moto. Kiporo ni chakula cha jana. Uji umepikwa leo(sijawahi kunywa uji wa  jana). Na kwetu, kiporo cha ugali wa muhogo hakipashwi moto; anapewa mtoto vile vile cha baridi, lakini uji anapewa wa moto. Kwenye hii blogu, nitaleta habari za jana—hizo ni ladha unazokumbuka, tena zingine zinakuudhi. Lakini nitatia na ladha za leo—huo ndio uji.
Kwenye kile kikao cha bloggers mimi ndio nilikua mtu mwenye furaha zaidi. Kwa vile bloggers wengine wote hawakuhudhuria, zaidi ya Pernille (duniaduara na Biche (wa chickabout town). Hivi wangekuja na wengine wote(nasikia wangefika zaidi ya 20) ningesema mimi ni nani—sharti kubwa la kuwapo pale ni kuwa na blogu. Nakumbuka alifika dada mmoja. Alisalimia, huku akitaja jina lake na blogu yake. Yaani kama vile niseme jamani habari zenu, samahani kwa kuchelewa. Naitwa Mkama, halafu naweka pause kidogo namalizia—kiporobaridiujimoto.
Niliona uso wa Pernille na Biche unawanda kwa tabasamu kisha wanasema kama kiitikio, ‘oohh, ndio wewe, karibu sana. Karibu kiti.’ Mimi wakati huo nilikuwa nimesahau hata neno la siri la kuingilia kiporobaridiujimoto.
Baada ya kikao nikaapa kwenda kuifungua tena blogu yangu. Nilijiwekea nadhiri kuwa iwapo kweli nikikaa mbele ya kompyuta na kukuta nimesahau password ya blogu yangu basi naachana na hii biashara maisha yangu yote.
Utakuwa unajiuliza nitakua na blogu kuhusu nini? Ah kwani hapa kwenye hizi aya unasoma kuhusu nini? Jibu lako utaniandikia kwenye kiboksi cha maoni hapo chini. Lakini hivi ni nchi gani ambako raia wake wakiulizwa swali nao wanajibu kwa swali? Tanzania? Kwani we unafikiri ni wapi kwingine ambako wakiulizwa swali wanasema tena swali? Si Tanzania tu?
Kuhusu nini cha Tanzania nitablogu. Vingi tu, lakini mizania itakua moja---mbadala. Napenda kuwaza mbinu mbadala, hoja mbadala, utatuzi mbadala, kila kitu mbadala. Naamini vitu hutokea kwa jozi kinzani. Kama kuna maji basi barafu imeyeyuka, mvua imenyesha ama chemichemi inavuja. Na kama unaona maji, basi umesiama pakavu. Na kama umesimama basi hujakaa.
Hii ni rahisi eh, ndio. Lakini mara nyingine giza isi jeusi, laweza kuwa jeupe.
Basi laiti kama kungekuwa mbinu mbadala ningejaribu kujua nini ungependa kusoma halafu ningeandika hicho tu. Lakini kwa vile si rahisi kutabiri, basi karibu ukae nami upwaani kwani ilishasemwa na kuthibika kuwa, mgagaa na upwa….
Haina mbadala hiyo.
Karibu tena

No comments:

Post a Comment