November 21, 2011

Naitabiria nchi yangu mabaya, lakini kinga na dawa ipoTanzania inapitia kipindi cha muhimu sana katika historia yake. Si tu sababu kutimiza miaka 50 tangu kupata uhuru na kuondokana na uwepo wa watawala wa kikoloni. Matukio yanayotokea yanaashiria aina nchi ambayo iko katika mpito.
Nchi hii inatoka kipindi ambacho raia wake waliweka imani yao kwa viongozi. Na sasa inaenda kipindi tofauti, zama za kuamini mfumo. Haina maana viongozi si tena wa muhimu, la hasha. Wala kuamini viongozi zamani haikumaanisha mifumo haikuwafaa. Kinyume chake,mtazamo wangu kwa kinachoendelea sasa ni watu wanaotaka kwanza mfumo, kisha ndio wamtafute mtu atayeufuata kuwapatia mahitaji yao.
Mtazamo  huu ndio unanituma kujenga rai kuwa, mabaya yanaweza kutokea. Iwapo waendeshaji wa mifumo ya kisiasa, kijamii na kiuchumi waliopo hawatajua cha kufanya na wakati bora wa kukifanya. Iwapo wawasilishaji wa maamuzi ya viongozi na matokeo ya uendeshaji wa mifumo iliyopo hawatawasilisha taarifa na maarifa kwa wakati na kwa ufasaha basi mabaya yanaweza kuikuta jamii hii illiyozoea amani.
Kuna viashiria vichache ambavyo si vigeni katika macho na masikio ya watu nataja baadhi yake na kuvihusisha na utabiri wangu.
1.   “Sina kabila, najua haki yangu, naidai na wenzangu”
Watanzania wanazidi kujitambua  na kujikusanya kwa maslahi yao. Hili ni jambo zuri. Badala ya kujitambua kama wakurya ama wagogo, kama wahindi ama wazungu watanzania wanaitana wafanyabiashara, wakulima, wafugaji wa kuhamahama, waalimu, vijana, wanafunzi(ama wanavyuo) na orodha hii inaendelea. Katika kujitambua huko wanadai haki zao na kuitaka Serikali iwatimizie wajibu wake kwao. Waalimu wana madai yao, wakulima wana madai yao, wafanyabiashara wana madai yao. Na ni ya haki, mara nyingi.
Nitoe mifano. Majuzi vyombo vya habari viliandika kuhusu wakulima wa Korosho mikoa ya Mtwara na Lindi wakiwakilishwa na jukwaa la wakulima wa korosho wakidai matokeo ya ahadi za Serikali kutatua tatizo lao la soko la korosho. Serikali ilipiga marufuku wanunuzi waliokuwapo, lakini haijatoa ufumbuzi wa soko la linalotoa bei inayomfaidia mkulima. Wakulima pia walijiunga huko Biharamulo na kushiriki kuwakamata watendaji waliohusika kuhujumu ufanisi wa matumizi ya vocha za pembejeo.
Miito ya kudau maslahi ya chama cha waalimu si migeni. Wafanyabiashara wana umoja wao. Mitandao hii inaongezeka. Aghalabu hujikuta wakiwa na maslahi na madai yanayofanana. Iwapo hakuna kingine kinachofananisha maslahi yao, basi wote ni walipa kodi.
2.   Mchakato wa katiba ndani ya Tanzania iliyoerevuka, yenye mitandao
Ni rahisi kuwaongoza wajinga na kutekeleza maono yako. Ni changamoto na pengine si vigumu kuwaongoza watu wanaojua kila unachojua. Na, ni vigumu kufanikisha maono yako-uliye kiongozi-iwapo unaowaongoza watu wanajitambua kwa namna tofauti.
Kuna zaidi ya magazeti 20 yanayochapwa nchini Tanzania. Kuna vituo vya televisheni zaidi ya 20 vinavyorusha matangazo yake ni 7 vinarusha matangazo nchi nzima—ongeza mamia ya televisheni za nchi za nje zinazotizamwa hapa nchini. Watumiaji wa mitandao ya kijamii wanaongezeka kwa kasi kila kukicha. Bei ya kutumia intenet inazidi kushuka(taratibu). Redio zinazorusha matangazo yake, na kusoma hewani magazeti hazipungui hamsini. Watanzania wasiokwenda shule, hata wale wasiojua kusoma  hawajawahi kuwa maarifa kama walivyonayo sasa. Leo mbunge akisinzia bungeni wapiga kura wake wanaweza kumjadili tangu saa hiyo hiyo wakimwona live.
Umbea hausubiri mbea afike. Kujua walivyofanya nchi za jirani hakusubiri habari zilizochujwa na gazeti teule. Hawa ndio watu ambao wanahitaji katiba mpya. Subira yao fupi,wako radhi kuiga mbinue zilizozaa matunda kwingineko. Wanafuatilia wanaharakati na wanasiasa wakiongelea katiba mpya. Mara moja wanachagua upande wa kuunga mkono. Kisha wanajadili na wenzao kwa hoja za ushawishi kama wao ni wasomi wa sheria. Wanashabikia wanayempenda, aliyekuna hisia zao, anayesema yanayogusa mahitaji yao. Kwa ufupi, wanajua wanachokosa.
Tayari wanajua katiba si ya chama cha siasa. Baadhi yao wana mashaka na uwezekano wa rais kuwaamulia wasivyopenda.  Yeyote mwenye mamlaka ama ushawishi wa kutengeneza mfumo wa kujua watanzania wanataka nini kingie kwenye katiba, ajue jambo moja kubwa. Watanzania wanasubiri kuona katiba inaelekeza kuhusu  mambo yote muhimu yanayohusu maisha yao.
3.   Migomo ya wanavyuo
Nimeamua kuziongelea harakati za hili kundi kwa upekee sababu zifuatazo. Tofauti na wakulima na wamachinga,  wanavyuo hupambana kutafuta haki zao huku wakiwa na nafasi kubwa zaidi ya kujikuta wao ndio watoa haki wa miaka ijayo.. Wanafunzi wa mwaka wa kwanza wanapofanya mgomo kudai nyongeza ya mikopo ya kusomea ama mazingira bora ya chuo, pia wanajua (ama kuota) si muda mrefu ujao na wao watakuwa ni waajiriwa wa taasisi ile ile waliyokuwa wakipambana nayo. Na ndani ya miaka 10 baadhi yao watakuwa na nafasi za kufanya maamuzi katika taasisi hizo. Pia kumbuka kuwa kundi hili linawekewa matumaini na jamii iliyo nje ya mfumo wa elimu. Wazazi wao na ndugu zao wanaamini kuwa kuna jambo wameenda kujifunza. Linalowakera lazima linafika na litaeleweka kwa umma mkubwa wa Tanzania hata kama halitaeleweka basi litagusa hisia zao. Uliza mianzo ya wanaharakati wanaouvuma katika jamii kwa sasa.
4.   Divai mpya, vibuyu vya zamani
Bado kuna sheria na taratibu ambazo hazijabadilika kulingana na mazingira ya kiribeali ambayo ndiyo nchi yetu inagamba kufanya kazi ndani yake. Lakini pengine hizo si shida kubwa. Utamaduni wa ufanyaji kazi ndio kilichobaki nyuma. Utamaduni wa kikazi ndani ya taasisi kama jeshi la polisi bado unatitisha mzani kupendelea Serikali. Huu ni urithi toka siasa za mrengo wa kisoshalisti. Inawezekana sheria zimebadilika lakini watendaji bado wana utamaduni wa zamani.  Aghalabu mabishano na kadhia baina ya polisi na watu wanaopita mitaani kwa mafungu makubwa wakidai kwenda kwenye mikutano inatokana tu na kuwapo kwa sheria na taratibu zinazotoa mamlaka kwa dola kukubali ama kukataa mikusanyiko. Kwa sababu nzuri tu, ni vizuri kuwapo uratibu na ulinzi wa usalama, lakini pia kadri watu watanzania wanavyozidi kujitambua kwa makundi na vyama vya kisiasa inazidi kuwa vigumu kutenganisha kati ya mkusanyiko watu wenye ajenga moja na mkutano wa hadhara usio na kibali.
5.   Nani anajua watanzania wanapenda ugali
Laiti nchini kwetu kungekuwa na taasisi (huru) inayoweza kufanya utafiti na kujea kwa uhakika maoni ya watu wengi kuhusu jambo fulani. Ingekuwa hivyo asingekuja mtu fulani akasema anatoa maoni ya wananchi wakati anatoa maoni ya kikundi chake tu. Wasingejitokeza wengine na kusema kwa vile wamechaguliwa basi wao ndo wana haki ya kusema, kisha kubatiza kila wanachosema kuwa ni matakwa ya wananchi. Kila anayesema anawakilisha maoni yetu, angetoa takwimu.
Mara nyingi mwanasiasa ama bidhaa, ama mtu mwenye umaarufu katika jamii akisoma takwimu hizo huzifanyia kazi mara moja. Nathubutu kusema hapa kwetu hata taarifa za vyombo vya habari  haziamiwi ama haziaminiki. Kiongozi hujisifia maarufu kwa umati uliokusanyika kwenye mkutano wake wa hadhara. Na kama kuna kiongozi asiyeitisha mkutano wa hadhara basi wengine hufikiri hana anayemuunga mkono.
Nchi zingine zina taasisi za kusoma umaarufu wa viongozi, vyama hata bidhaa. Maoni hayo hutolewa kwa mtandao, ama simu. Yakikusanywa hutolewa hadharani kwa haraka na kwa wakati ambao ujuzi huo unahitajika. Kuna vyombo vya habari kama mwananchi, New Habari vinaitisha watazamaji wa tovuti zao kupiga kura kuhusu maswala wanayochagua wao. Ni mwanzo mzuri, lakini matokeo hayatangazwi,na wanaopiga kura ni wachache, toka katika 5% ya watanzania wanaopata mtandao. Taasisi ya Uwazi imeanzisha wananchi survey, ambayo itachukua maoni nchi nzima, pengine kutakuwa na jipya hapa.
Kabla hatujapata namna ya kujua maoni ya watu wengi, bado kila anayefikiri anao ushawishi kwa umma atasimama na kusema anajua mawazo yetu.
6.   Siasa kwa kila jambo
Ndio, utashi wa kisiasa ni muhimu ili kuanzisha mchakato wa suala linalohusu jamii. Lakini si salama kama miwani ya siasa itatumika kutazama kila jambo. Yapo ambayo yanahitaji taaluma na lazima yajulikane hivyo na yaheshimiwe. Afya inahitaji daktari na kanuni za afya, maji yanatakiwa kuwa safi kwa kila mtu ili ayanywe. Na, uchumi ili ukue unahitaji uzalishaji ukue. Nilicheka majuzi niliposikia wanasiasa wanajaribu kumweka kiti moto waziri wa fedha na gavana wa benki kuu kwa kushuka kwa thamaniya shilingi dhidi ya dola ya Marekani.
Ni kweli hao wanalo la kufanya, lakini kama hatuzalishi, siasa zetu hazitaweza kututengenezea uchumi. Kama siasa haiewezi kuhakikisha kanuni za kitaaluma zinafuatwa basi wanaoendesha siasa hawana haki ya kuendesha siasa zao kutokana na mapato ya uchumi huo. Kwa kuwa siasa zimekua ndio fungate ya kila jambo linalotajwa katika nchi yetu, sasa jamii yetu imejikita katika laana nyingine nayoitaja hapa chini. Utagundua siasa imeteka nyara taaluma pale mambo ya kitaalamu yanapoundiwa tume, kinyume na kutumia nidhamu ya kazi na kitaaluma kuadhibu uzembe na kutowajibika.
7.   Rushwa-motisha ufanisi na malipo yanayotabirika
Rushwa ni sekta mojawapo ambayo inatabirika na inazalisha mapato ya uhakika kwa maofisa wa serikali na wafanyabiashara. Kwa wanyonge wanaofikiri kupata haki zao bila kutoa malipo ya ziada rushwa ni kizingiti kinachojulikana. Sio siri. Rushwa ni kigezo cha wahitimu kuchagua kazi fulani na kwa wafanyakazi kuacha kazi Fulani na kufuata kazi nyingine. Rushwa ni kigezo cha matumaini kwa watumishi wanaolipwa ujira mdogo. Ni chanzo cha kikuu cha kipato kwa madalali wanaojua nani wa kumpa rushwa ili mambo yaende. Rushwa, narudia tena, ndio sekta inayotabirika kuliko zote, huduma iliyo bora, na malipo ambayo mwenye kuhitaji huduma anajiandaa kuyatoa kabla ama baada ya kupata huduma ambayo ni haki yake. Ni bakshishi ambayo mpokea huduma asipotakiwa kuitoa anaona amenyimwa haki ya kulipa ‘fadhila’ na pengine anajiona hakufanya jambo la utu. Rushwa inajenga undugu baina ya watu ambao pengine wangeishia kusabahiana kwa juu juu tu katika masaa ya kazi. Lakini pia ni kigezo cha wengine kufunguliwa mlango na wengine kufungiwa—na kila mmoja anakubali kuwa lililomkuta ni staili yake. Aliyefungiwa anajilaumu mwenyewe kwa kukosa kibakshishi cha kutoa, anayefunguliwa anaona amefanya wajibu unaostahili. Natabiri mabaya kwa nchi yangu kwa kuwa kila mtu anatoa na kupokea rushwa na hakuna anayeikemea wakati inapotakiwa kutolewa.


Dawa  na kinga ndani chembe hai za ugonjwa

Wataokomesha rushwa ni wala rushwa na watoa rushwa. Watakaotenga siasa na taaluma ni wataalamu na wanasiasa(na wataalamu walio pia wanasiasa). Makundi ya kijamii yatakayoleta amani ni yale yatakayoendelea kudai haki zao na uwajibikaji kwa Serikali bila kukoma na bila kutumia mbinu zinazovunja amani. Na, cha muhimu zaidi. Serikali inayotakiwa kusoma alama za nyakati, kutambua mahitaji ya watu wake na kujizatiti kuona yanafanyiwa kazi ni hii iliyo madarakani.  Awamu hii ya uongozi wa taifa inayo fursa ya kufanya mambo ambayo, kamwe, awamu zingine zote zilizopita na zijazo hazitapata fursa ya kuyafanya. Si sahihi kuilinganiza zama ya urais na uongozi mzima wa Tanzania ya sasa na nyingine yeyote. Hii ni maalumu, na kama haitaacha urithi maalumu basi, bado itaacha ombwe la pekee yake kwa sababu fursa itakuwa imepita ya kuyafanya mambo maalum, kwa namna maalumu kama ambavyo inawezekana sasa.No comments:

Post a Comment