November 8, 2011

Linahitajika Azimio Lingine toka Arusha

TUNACHOKIONA Arusha kwa sasa  ni zaidi ya siasa. Vyama viwili vya siasa vyenye nguvu kubwa hapa nchini vya CCM na CHADEMA  kila kimoja kinachakujivunia nguvu ambayo kingine hakina. Kwa upande wa CCM kinajivunia nguvu ya Dola huku chama cha upinzani  cha CHADEMA kinajivunia nguvu ya umma.

Na ndicho  kinachopelekea  mvutano usioisha tangu kufanyika kwa uchaguzi mkuu mwaka jana Octoba 30 mpaka leo. Arusha imekuwa ikiendelea na mivutano ya kisiasa kana kwamba   uchaguzi umnekaribia ilhali bado kuna safari ya miaka 4  mbele.

Nachelea kutoa hofu yangu kuwa iwapo vyama hivi vitaendelea kutunishia misuli yao: CCM nguvu ya dola, Chadema nguvu ya umma, vitazidi kuigawa Arusha kwa misingi ya kisiasa, na haitaishia hapo. Kumbuka wakati wa uchaguzi kulikuwa na tetesi za kidini katika siasa za Arusha. Iwapo siasa za jukwaani zitazidi kushikilia mitaji ya kila chama, bila kutafuta suluhu tusishangae siku nguvu ya umma ikipambana tena na nguvu ya dola mitaani.

Dkt Slaa, katibu Mkuu wa Chadema na Tundu Lissu, mnadhimu wa kambi rasmi ya upinzani bungeni walikamatwa  Novemba 8 majira ya asubuhi  Arusha wakiwa katika harakati za kushinikiza kuachiwa toka rumande katika gereza la Kisongo Bwana Godbless Lema, Mbunge wa Arusha Mjini. Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, pia anatafutwa kwa tuhuma hizo. Mbunge wa jimbo la Arusha mjini,  Godbless Lema, awali alikataa dhamana katika shtaka analokabiliwa nalo yeye na wafuasi wengine kwa kuandamana  na kufanya kusanyiko bila ya kibali kutoka Jeshi la polisi.

Huu ni mwendelezo wa siasa za Arusha, ambazo zinazidi kuvaa utambulisho wa ghasia. Kwa hiyo ninalo jibu la swali langu la kwanza. Kinachoendelea Arusha ni siasa za ghasia.
Katika mazingira kama hayo, kujikita katika shughuli za maendeleo ni nadra. Bado baraza la madiwani halijatulia. Ni baraza hili ambalo ndilo linatakiwa kukaa na kufanya maamuzi muhimu ya namna ya kufanya shughuli za maendeleo ya jiji la Arusha. Haya hayawezekani kama madiwani wa vyama vyote bado wanahaha kutafuta suluhu na nafasi za kulipa visasi vya kisiasa. Chadema wanadai uchaguzi mpya wa meya.

Mapambano ya siasa za Arusha yana sura kadhaa.  Kuna mapambano baina ya vyama na kuna mapambano baina ya makundi ndani ya vyama.
Madiwani wa Chadema walivuliwa uanachama kwa tuhuma za kuingia muafaka na chama pinzani na baadhi  yao kupata nyadhifa katika baraza la madiwani la jiji, kinyume na utaratibu wa chama chao.
Walijaribu kujiokoa kisiasa  kwa kwenda mahakamani , lakini mpango wa suluhu kwa njia ya sheria ukakwama kwa shauri lao kupigwa chini na mahakama. Pengine salama yao ni kujisalimisha kwa taratibu za chama chao.

Hayo ni ndani ya Chadema. Upande mwingine wa migogoro ni  ndani ya CCM. Viongozi wa vijana wa CCM walifika Arusha na wakaendesha mikutano ya kisiasa ya ndani ya chama. Na waliitisha mikutano ya hadhara bila kupata kibali cha walinzi wa usalama, yaani jeshi la polisi.
Kundi lingine la wanachama lilidai mikutano illiyoitishwa na hao viongozi  wenzao wa UVCCM (taifa) si halali na haikuwa na maslahi ya chama.

Ikasikika sauti nyingine ikisema ni watoto wa vigogo ndio walioamuru mikutano hiyo ifanyike, kinyume na utaratibu. Bila shaka sasa inaonesha siasa za Arusha, zinaweza kubainisha mipasuko katika chama, hata kama ingekuwa imesitirika katika siasa za Dodoma na Dar es Salaam.
Kuna sura nyingine, pengine muhimu zaidi ,ya siasa za Chadema na CCM zinapofika Arusha. Vyama vyote vinatafuta kuimiliki Arusha. Chama cha Mapinduzi kilishinda urais, hivyo kinashikilia na kuendesha dola. Chadema kilishinda kiti cha ubunge Arusha, hivyo kinajinadi kwa kuwa na idadi kubwa ya wafuasi na wapiga kura wanaokiunga mkono mjini arusha. Kwenye viti vya udiwani CCM ilipata 10 na CHADEMA ilipata 8 huku TLP ikiambioia kiti kimoja.

Kila chama kiliona kina haki na nafasi ya kuwa na udhibiti wa baraza linaloongoza jiji. Ndipo kilipo kitovu cha ugomvi  baina ya vyama hivi na mivutano ya ndani ya kila chama. 

Kwa upande mwingine kuna jeshi la polisi. Sikusikia nidhamu waliyopewa viongoziwa UVCCM pale walipofanya mikutano bila kibali jijini Arusha, lakini mbunge wa Arusha aliwekwa rumande kwa kosa la kufanya mkusanyiko wa hadhara bila kibali cha polisi. Watu wanasikia, wanafuatilia, na bila shaka na wanasiasa wa  chadema wanatumia fursa hizo kuchochea nguvu ya umma, wakijua dola inafanya kazi kwa upendeleo.

Natarajia hivi karibuni kusikia mkutano utakoitisha Azimio jipya la Arusha ili kuwepo na haki, amani na jitihada zenye tija kwenye siasa za Tanzania, kwa kuanzia Arusha.
 Tumefika ama bado?


No comments:

Post a Comment