December 1, 2011

Kazi yako ina maslahi?


Kazi yako ina maslahi? Niliulizwa na rafiki yangu mmoja hivi karibuni wakati tunabarizi uswahili kwetu tukijadili mwenendo na mustakabali  wa maisha tunayoishi.
Nikajibu, ndio, kisha nikataja mshahara naopata.
"Ah, hapana. Nasema, yaani, pesa," alijibu huku akinyoosha mbele yangu mkono na  kusuguasugua dole gumba lake kwenye ncha za vidole vingine.
Nikajibu, "Ndio mshahara naopata ni pesa, silipwi chakula." huyu jamaa huwa ana kawaida ya kuuliza maswali tata.
"Naona hujanielewa," alisema tena, na sauti yake ikiungana na sura yake kunishangaa.
Kweli sikumwelewa mapema.Mimi nilielewa kuwa maslahi ni mshahara unaopata mwisho wa mwezi baada ya kufanya kazi. Hivyo, jibu la swali lile pale barazani kama angeendelea kunighasi ningemwambia mshahara naopata unatosha, ntafanyaje sasa.
“Unajua kuna kazi zingine zinakuwa na mshahara mdogo, lakini zinakuwa na marupurupu mengi,” alianza kutoa muhadhara. Nakubali yeye ni mjuzi wa mambo ya aina hii zaidi yangu. Akaendelea kufafanua; kwamba kuna wafanyakazi wanalipwa shilingi laki moja tu, lakini pale wanapofanyia kazi kuna uwezekano wa kupata mishiko ya hapa na pale hadi wakijumlisha kwa mwezi mmoja wanaweza kutengeneza hadi laki 3.
Si huyu tu anayeongelea maslahi namna hiyo. Nilipoanza kuvumbua maana ya maslahi nilikumbuka kuna mengi nilishasikia. Mwingine alinilaumu kuhusu kazi niliyoiomba kisha nikaikataa baada ya kugundua mshahara wake ni mdogo. “Umechemsha wewe,” alinambia huku akitupa mkono hewani kuashiria ujuha wangu.
“Ni kweli ile kazi mshahara kidogo. lakini pale kuna visafari na visemina vya hapa na pale. Kwa maelezo ya mzoefu huyu, kwenye hiyo ofisi wafanyakazi wakifanya mkutano kwenye ukumbi wa ofisini kwao wanapata pesa. Wakienda nje ya ofisi yao, wakiwa mji ule ule, wanapata posho. wakisafiri…”
Nilifafanuliwa maslahi mengine na yule rafiki yangu wa pale barazani. “Kuna kupata chakula cha bure ofisini, semina, kwenda kuhudumia mabosi wakienda kwenye mikutano nje. Zote hizo ni nafasi za kupata pesa nje ya mshahara,” alisema rafiki yangu, ambaye hufanya kazi ya uhudumu wa ofisi.
Kufikia hapo nilianza kupata mashaka kama kazi yangu ina maslahi. Lakini naipenda, na nikipata pesa mwisho wa mwezi najisikia raha na natumia na kupanga maendeleo yangu. Na, si ndio malipo nilikubaliana na mwajiri wangu!
Niliamua kuweka swali hilo kwenye ukurasa wangu wa facebook. Majibu yakaja. Rafiki mmoja alinitafsiria hata swali lenyewe (kazi yako ina maslahi), aliandika: Je, kuna pesa ya ziada zaidi ya mshahara? (Zile nje ya haki yako stahili) - kuna uwezekano wa kuandaa malipo hewa, wizi wa mali ya ofisi, mafuta ya gari hewa, vipuli hewa, stationery hewa nk nk nk.....
Kwa kazi nayofanya, mezani kwangu kuna kompyuta na nachozalisha ni karatasi zenye sentensi nyingi na machapisho. niliposema machapisho, mmoja akaniuliza, kwani hupeleki kuchapa viwandani? Hapana, nilisema na kutikisa kichwa. “Okay, basi hapo huwezi kutengeneza pesa,” alisema kuashiria mwisho.
Siku mbili zilizopita nilisoma muendelezo wa mjadala mrefu kuhusu posho za wabunge. Najua wanapata mshahara unaofikia Tshs mil 7. Lakini wanaona hazitoshi. Kumbe, wanayo pia mapato nje ya mshahara. Posho za vikao. Wabunge, ambao wanalipwa mshahara kwa kutuwakilisha bungeni(ndipo ofisini kwao), wanalipwa pesa nyingine kwa ajili ya vikao. Loh. Hivi maelezo ya kazi ya mbunge ni nini? Hivi bungeni Dodoma si mahala pa kazi pa mbunge?
Maswali ninayo mengi. Baadhi yameshajibiwa na aliyenicheka kwa kukataa kazi kwenye ofisi ambayo huwa wanawalipa wafanyakazi wao kwa kuhudhuria vikao na semina ndani ya ukumbi wa mikutano wa ofisini kwao.
Kwa vile nimechagua kufanya kazi, basi nitaendelea. Swali nililo nalo binafsi ni kama nina haja ya kutafuta kazi yenye ‘maslahi.’
Nimeshaziona kadhaa, kama ubunge. Rafiki yangu mwingine anayefanya kazi ambayo haina maslahi pia anasema ameanza utafiti ili apate yenye maslahi. Na sehemu mojawapo ya utafiti wake ni kwenye televisheni. Anaangalia ni taasisi zipi huandaa semina na warsha mara kwa mara na kuita wanahabari kupiga picha wajumbe wakiwa katika meza ndefu, wakiwa na chupa za maji mbele yao wakisikiliza wawezeshaji wakitoa mada. “Huko lazima kuna maslahi,” anasema kwa uhakika.
Mimi nimeamua kufanya uamuzi tofauti. Niliuandika kwenye ukurasa wangu wa facebook, rafiki mmoja akajibu ni kama najiua mwenyewe. Nauliza na kwako mwenzangu, kazi unayofanya sasa ina maslahi?






No comments:

Post a Comment